New Jersey - USA
Mwanaume mmoja kutoka New Jersey ameshtakiwa kwa kosa la kumdunga kisu
mchumba wake hadi kufa, siku moja tu baada ya kuposti video ya posa yake kwenye
Facebook.
Jose Melo, mwenye umri wa miaka 52, anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya
kiwango cha kwanza na kumiliki silaha kinyume cha sheria kufuatia kifo cha
Naket Jadix Trinidad Maldonado, mwenye umri wa miaka 31, kama ilivyotangazwa na
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Union nchini Marekani.
Polisi waliitwa nyumbani kwa Melo, mjini Elizabeth, muda mfupi baada ya saa
tatu asubuhi Jumatatu iliyopita, na walikuta Maldonado amekufa eneo la tukio.
Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, lakini lilitokea siku moja tu baada
ya Melo, DJ wa eneo hilo, kuposti video ikionyesha akimposa Maldonado hadharani
katika Klabu ya Usiku ya Bamboleo, kwa mujibu wa ripoti za Fox 5.
Katika video hiyo, Melo alionekana akipiga goti moja chini na kumwambia
Maldonado, “Te amo,” maneno ya Kihispania yanayomaanisha “Nakupenda,” huku
akifungua sanduku la pete. Maldonado alionekana kushangazwa na posa hiyo, akiwa
amebakia mdomo wazi kabla ya kusogea na kumbusu Melo, ambaye aliendelea
kumvalisha pete hiyo.
Wawili hao walikumbatiana huku umati wa watu ukishangilia, na wimbo “Casate
Conmigo” (Uolewe Nami) wa Silvestre Dangond na Nicky Jam ukisikika
ukipigwa kwa nyuma.
“Nakupenda, mpenzi,” Melo aliandika kwenye chapisho la Facebook.
Ripoti zinaonyesha kuwa Melo aliwahi kukamatwa mwaka 2010, baada ya
kumtishia mwanamke mmoja kwa kisu cha kukatia maboksi na kumbaka. Kisha
alilazimishwa kujiandikisha kama mkosaji wa makosa ya kingono, na orodha ya
serikali ya New Jersey inamtaja kama mkosaji wa kiwango cha pili, ambaye ni
hatari ya wastani.
Haijulikani jinsi Melo alivyokutana na Maldonado au walichumbiana kwa muda
gani kabla ya posa hiyo, lakini ukurasa wa kuchangisha pesa mtandaoni umeelezea
kuwa mwathiriwa alikuwa mama wa watoto wawili wa kike.
“Naky alichukuliwa kikatili kutoka kwetu mnamo Desemba 30,” shangazi yake
aliandika kwenye GoFundMe. “Kitendo hiki kibaya kilichofanywa na mtu
aliyemwamini kimewaacha watoto wake wawili bila mzazi yeyote na bila chaguo
nyingi za maisha ya baadaye.”
Aliongeza kuwa binti za Maldonado wako salama na wanatunzwa na familia, huku
mipango ya kudumu ikiandaliwa.
Mazishi yatafanyika New Jersey na Florida, na mwili wa Maldonado utazikwa
katika nchi yake ya asili, Puerto Rico.