Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit
Kombo, amesema kuwa Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la mwaka
2024) inalenga kuiimarisha Tanzania kimataifa kwa kutumia diplomasia makini na
shirikishi ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa.
Akizungumza leo Jumatatu, Mei
19, 2025, katika uzinduzi wa sera hiyo uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano cha Julius Nyerere, Balozi Kombo amesema Tanzania ina dhamira ya
kuendelea kuwa kisiwa cha amani, utulivu na umoja, na kuwa na mchango mkubwa
katika ulinzi wa amani duniani.
“Sera hii ni nyenzo ya
kimkakati kuhakikisha Tanzania inaendana na mazingira yanayobadilika kwa kasi
duniani, huku ikiimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa tija zaidi,” amesema.
Waziri Kombo amefafanua kuwa
sera hiyo inaiwezesha Tanzania kuwa na sauti yenye ushawishi katika uhusiano wa
kibiashara na kimataifa, sambamba na kuchochea ushiriki wa nchi katika masuala
ya kiuchumi duniani.
Aidha, ameeleza kuwa mchakato
wa maboresho ya sera hiyo ulihusisha ushiriki mpana wa wananchi kutoka maeneo
mbalimbali nchini, kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, jambo
linaloifanya kuwa sera shirikishi na jumuishi.
“Ni matarajio yetu kuwa malengo
yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ikiwemo kufikia uchumi wa
kipato cha kati cha juu, yatatimia kwa kutumia sera hii kama mwongozo wa
kimataifa wa utekelezaji,” amesema Balozi Kombo.
Sera hii mpya inajengwa juu ya
msingi wa kulinda maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia
mazingira ya sasa ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiusalama katika ngazi ya
kikanda na kimataifa.