WENYEJI, Yanga wameweka hai matumaini ya kufuzu
Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa Kundi A
jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Haikuwa ushindi mwepesi kwa mabingwa hao wa
Tanzania, Yanga baada ya TP Mazemba, mabingwa mara tano wa michuano kuanza
kupata bao dakika ya 16 likifungwa na kipa Msenegal, Alioune Badara Faty
kwa penalti kufuatia beki Mkongo, Chadrack Issaka Boka kumchezea rafu beki wa
Kimataifa wa Mauritania, Ibrahima Keita mzaliwa wa Mali.
Ikawa siku nzuri kwa mshambuliaji mzawa, chipukizi
wa umri wa miaka 20, Clement Francie Mzize aliyefunga mabao mawili dakika
ya 33 na 60, huku bao lingine la Yanga likifungwa na kiungo wa Kimataifa wa
Burkina Faso, Stephane Aziz Ki dakika ya 56.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi nne na
kusogea nafasi ya tatu, ikiishushia nafasi ya nne TP Mazembe inayobaki na
pointi zake mbili baada ya wote kucheza mechi nne.
Al Hilal Omdurman inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake
tisa, ikifuatiwa na MC Alger yenye pointi nne na wastani mzuri wa mabao zaidi
ya Yanga baada ya wote kucheza mechi tatu.
Saa 4:00 usiku wa leo Al Hilal Omdurman watamenyana na MC Alger Uwanja
wa Cheikha Ould Boidiya Jijini Nouakchott nchini Mauritania katika mchezo wa
nne baina yao wa kundi hilo.
Ahmedabad