Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imefanya
ziara ya ukaguzi na Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Radiolojia Mkoani Njombe kwa
kutembelea vituo vipatavyo 32 ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Akizungumza jana Desemba 18 baada ya
kukamilisha zoezi hilo, Mkuu wa Kanda ya Kati, Bw. Machibya Matulanya
ameridhishwa na ubora huduma za Radiolojia kwa vituo vilivyopo Nyanda za Juu
Kusini, ikijumuisha mikoa ya Njombe, Iringa, pamoja na Ruvuma.
"Kwa zaidi ya asilimia 80 ya vituo
tulivyotembelea katika Ukanda huu vimekidhi mahitaji ya kitaifa ya usalama wa
mionzi na asilimia 20 ya vituo tulivyopitia vimekuwa na changamoto mbalimbali
ambazo zinahitaji marekebisho ya haraka." Amesema Bw. Matulanya.
Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa
kufanyiwa ukaguzi Mkoani Njombe yalihusisha ukaguzi wa Mashine za X - Ray za
kawaida, X - Ray za Kinywa na Meno, Mashine za CT Scan, MRI, na mashine za
Viwandani.
Ametoa wito kwa mafundi sanifu wa vifaa
vya Atomiki kuwa na leseni kwa kuzingatia sheria ya nguvu za atomiki kifungu
cha 25.
Ameasa pia taasisi zinazonunua vifaa
vipya vyenye nguvu ya Atomiki kuhakikisha vinasajiliwa, na kukaguliwa, pamoja
na kupewa leseni kabla ya kuanza kutumika.
Mratibu wa Huduma za Radiolojia Mkoa wa
Njombe, Bi. Eva Nathaniel Sijaona, ameomba serikali kuendelea kuajiri watumishi
katika huduma mionzi ili maeneo yaliyopata vifaa hivyo yaweze kutumika na
kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi,
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Lazaro Jassely ameahidi kuwa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kupitia wataalamu wake, itaendelea
kuwajengea uwezo wataalamu walio katika vituo vilivyopo chini yake, ikijumuisha
Hospitali za Halmashauri, Wilaya na vituo vya Afya.