Wataalamu wamewataka wananchi wa Uingereza kuwa makini na dalili za siri za
virusi vya human metapneumovirus (HMPV), ambavyo vimekuwa vikisababisha
taharuki nchini China na vinaendelea kusambaa Uingereza.
HMPV, ambavyo vinaathiri zaidi watoto, vimeibua ongezeko kubwa la maambukizi
katika majimbo ya kaskazini mwa China, na kusababisha hospitali kufurika
wagonjwa, hali inayofanana na siku za mwanzo za Covid.
Data za hivi karibuni nchini Uingereza zinaonyesha ongezeko kubwa la maambukizi
ya HMPV wiki za hivi karibuni, kiwango kilicho juu zaidi ikilinganishwa na
kipindi kama hicho mwaka jana.
HMPV mara nyingi husababisha dalili zinazofanana na mafua ya kawaida, kama
kikohozi, mafua, koo kuuma, na homa ambayo hupotea baada ya siku tano. Hata
hivyo, kwa baadhi ya watu, hasa walio katika hatari kubwa, virusi hivi vinaweza
kusababisha magonjwa makali kama bronchitis, bronchiolitis, au pneumonia, na
dalili kama kupumua kwa shida, kikohozi kikali, na sauti ya kugugumia.
Profesa John Tregoning wa Chuo Kikuu cha Imperial London ameeleza kuwa dalili
za HMPV, hasa kwa watoto, zinafanana sana na zile za RSV (Respiratory Syncytial
Virus). Virusi hivi husambaa kupitia kikohozi, chafya, na matone ya mate.
Ameshauri wananchi kulinda afya zao kwa kuhakikisha maeneo wanayokaa yana
hewa safi, kufunika mdomo wanapokohoa, na kunawa mikono mara kwa mara. Kwa
walioathirika, hatua muhimu ni kupumzika, kunywa maji mengi, na kujitenga ili
kuepuka kuwaambukiza wengine.
Tofauti na Covid, hakuna chanjo wala matibabu mahususi ya virusi vya HMPV.
Matibabu yanayopatikana ni ya kupunguza dalili tu. Wale wanaohisi hali zao
kuzorota wanashauriwa kumuona daktari, lakini wataalamu wameonya kuwa
antibiotiki hazina athari kwa virusi hivi.
Wataalamu wamebainisha kuwa ongezeko hili halipaswi kuzua hofu isiyo ya
lazima, lakini uangalifu wa ziada ni muhimu katika kipindi hiki cha baridi.