Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, ametaja umri, kufanya kazi muda mrefu serikalini na uwepo wa vijana wanaoweza kumsaidia Rais katika Majukumu ya Nafasi ya Makamu wa Rais ni kati ya sababu ambazo zimemsukuma kuomba kustaafu nafasi hiyo.
Akizungumza leo katika kikao kazi cha Tano cha Serikali
Mtandao, kinachofanyika ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha, Dkt. Mpango amesema
“Kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka
2022, asilimia 77 ya idadi ya watu nchini ni vijana; sasa Mimi nimetumika
serikalini kwa muda wa kutosha ….. bado nina nguvu, yapo mambo ambayo ninaamini
kwamba inahitaji nafasi kwa ajili ya kuchangia pato na maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa nafasi adhimu alizowahi
kutumika serikalini zinaweza kutumikiwa na watanzania wengine, hivyo uamuzi
wake unalenga pia kuacha nafasi ya watu wengine kutoa mchango kwa Taifa hasa
kwa nafasi alizohudumu.
“Ukipanda Treni ni muhimu kujua unapandia kituo gani, muda
gani na unateremka muda gani na kituo gani; la sivyo litakupitiliza. “Ninaamini
kuwa chaguo lililofanywa na chama chetu ni chaguo sahihi kabisa” amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amehudumu serikalini kwa nafasi mbalimbali ikiwemo Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa miaka 14, Naibu Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mtendaji Tume ya Mipango kwa Miaka sita (6), Waziri wa Fedha, Miaka mitano na miezi minne, Benki ya Dunia, Msaidizi wa Rais Kikwete - Ikulu, na miaka minne, akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania katika serikali ya Awamu ya Sita.
Amehimiza viongozi wengine kuona umuhimu wa kuwa na muda wa kutosha kuandika, ili kujenga kumbukumbu nzuri na historia ya Taifa la Tanzania.