Rais wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) Boniface Mwabukusi
ameshauri serikali na sekta binafsi kuendelea kushirikiana katika kusimamia na
kutekeleza sheria mbalimbali zilizowekwa ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia
watanzania.
Mwabukusi ametoa kauli hiyo leo Februari 3 ikiwa ni kilele
cha maadhimisho ya wiki ya Sheria duniani.
Katika Hafla hiyo inayofanyika jijini Dodoma, Mgeni Rasmi
akiwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwabukusi amenukuliwa akisema
“ Tunaposhirikiana na serikali hatulambi asali….TLS sio kikundi cha magaidi …..
sehemu ya kuonya tutaonya kwa haki, kupongeza tutapongeza kwa haki na yale ya
kushiriki kufanya kazi tutashiriki kwa haki kulijenga taifa letu na kumhudumia
mwananchi” amesema.
Pia amesisitiza kwa kusema “TLS tumekuwa tukizunguka kupitia
Mama Samia Legal Aid, na sisi tumekuwa tukishiriki mikoa yote kuwafikia
wananchi; kwahiyo kuptia program kama hiyo serikali inakuwa inatusaidia moja
kwa moja kwa sababu wananchi wengi wanaofikiwa na huduma ile ni wale wananchi
ambao hawana uwezo wa moja kwa moja wa kupata ile huduma ya mawakili kulingana
na uwezo wao kiuchumi na maeneo waliko”
Mwabukusi ameshauri sheria zinazotungwa, ziwe na ushirikishaji
wa maoni baina ya watunga sheria na wananchi ambao ndio watumiaji wa sheria hizo.
Mbali na hayo ameshauri kuboreshwa kwa maslahi ya mahakimu
kwa kile alichoeleza wao ndio wanaoshughulika na wananchi wa chini; hivyo kutokuwepo
kwa maslahi mazuri kunaweza kuwa chanzo cha upindishwaji wa haki za wananchi.