Klabu ya Soka ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe,
(Njombe RRH FC) inatarajia kuingia dimbani dhidi ya Timu ya Soka ya Hospitali ya
Kanda Mbeya (MZRH FC) Mchezo unaotarajiwa kuchezwa mnamo Aprili 5, Jumamosi
katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza jana Aprili Mosi, baada ya mazoezi ya kuendelea
kujiweka imara Kocha wa Njombe RRH FC, Admin Mashaka amesema anatambua ukubwa
wa Timu ya Hospitali ya Kanda Mbeya lakini wamejipanga kuhakikisha wanarudi na
ushindi katika mchezo huo wa Ugenini.
Naye Nahodha wa Timu ya Njombe RRH FC Peter Mwanjabala, amepongeza
mwitikio wa wachezaji, wapenzi na mashabiki wa Timu hiyo kwa kuendelea kujitokeza
katika michezo ambayo imekuwa ikiendelea ili kujifua zaidi kuelekea mchezo huo.
Amewataka mashabiki kuendelea kuchangia nauli ili kuongeza
nguvu ya mashabiki wa Njombe RRH FC watakaojitokeza kuipa nguvu timu hiyo, huku
akiahidi kuwa timu hiyo itajitahidi kurudi na ushindi.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Njombe, akizungumza pia kwa niaba ya Menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Njombe amesema kumekuwepo na ushirikiano mzuri na udugu wa kudumu kati
ya Hospitali hii na Hospitali ya Kanda Mbeya ikiwemo kuwajengea uwezo watumishi
wa Njombe RRH, hivyo uwepo wa mchezo huo ni mwendelezo wa ushirikiano na
kufahamiana miongoni mwa watumishi wa taasisi hizi mbili.
Pia ameushukuru Uongozi wa Hospitali kwa kuipa nguvu timu
hiyo kwa kufanya uwezeshaji katika maeneo mbalimbali yatakayosaidia kufanikisha
uwepo wa mchezo huo.