Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema uanzishwaji wa Benki ya Ushirika Tanzania ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na utekelezaji wa wazo la muda mrefu la kuhakikisha sekta ya ushirika inakuwa na benki kubwa inayoihudumia.
Rais Dkt. Samia
ameyasema hayo leo wakati akizindua Benki ya Ushirika Tanzania, katika Ukumbi
wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Benki hiyo itakayojikita kuchochea ufadhili wa mitaji zaidi
kwenye sekta ya ushirika inamilikiwa kwa 51% na vyama vya ushirika, 20% na
Benki ya CRDB, 10% na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na 9% na
wanahisa wengine.
Rais Dkt. Samia ameipongeza benki hiyo kwa kuanza vizuri
ambapo amesema “Mmeanza na mtaji wa Shilingi Bilioni 58, ni mtaji mkubwa, benki
haianzi kinyonge. Kiasi hiki kitasaidia kuongeza mitaji kwa wakulima kwa kutoa
mitaji na kuchochea kuongezeka chakula na mazao mengine ya kilimo nchini."
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa dhamira ya
Serikali ni kuona ushirika unaimarika na kuongeza mchango wake kwenye Pato la
Taifa na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Dkt. Samia amezitaka Wizara
ya Fedha, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kutafuta jawabu la changamoto ya upatikanaji mitaji katika sekta ya kilimo
nchini. Vilevile, Rais Dkt.
Samia ameiagiza Tume
ya Maendeleo ya Ushirika kusimamia vyama vya ushirika ili vijiendeshe
kibiashara na kuvitaka vyama vyote nchini kuimarisha uwajibikaji na uwazi.
Ameeleza kuwa matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa
ushirika, yatasaidia kujenga imani ya wanaushirika kwa vyama vyao.
Ahmedabad