Wataalamu watano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kutoka Idara ya Maabara na Kitengo cha Afya, Kinga na Mazingira wamejengewa uwezo katika ufuatiliaji wa magonjwa (Laboratory Based Surveillance) zoezi lililodumu kwa siku nne kuanzia Jumatatu, Mei 12 – 15.
Mafunzo hayo yameongozwa na wataalamu wawili kutokea Wizara Ya
Afya akiwemo Rais wa Chama cha Wataalamu wa Maabara (MELSAT) Bw. Yahaya R. Mnung’a
na Mlezi wa Maabara Kanda ya Mashariki, Bw. Hamza Matimba.
Akifunga mafunzo hayo Rais wa MELSAT alisisitiza wataalamu
wa Maabara kufanya kazi kwa kufuata miongozo iliyowekwa huku akiacha ujumbe wa
mshikamano na umoja miongoni mwa wataalamu hao.
Kwa upande wake Mratibu wa Maabara Kanda ya Mashariki
amesema kuwa Idara ya Maabara ni eneo nyeti na muhimu sana katika kugundua na kuthibitishwa
kwa milipuko ya magonjwa kwa haraka, hivyo akaasa wataalamu hao kuitumia
taalamu yao katika kuhakikisha taaluma yao inaleta tija kwa jamii.
Naye Mratibu wa Huduma za Maabara Mkoa wa Njombe, Bw. China
Mbilinyi, amewaasa wataalamu wa Maabara Njombe RRH, kuwa na tabia ya kujisomea
na kujiendeleza katika masomo ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika
maabara ikiwemo matumizi ya akili mnemba katika utoaji huduma za maabara.