Imeelezwa kuwa Tanzania haikuchaguliwa kwa bahati mbaya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, isipokuwa imekidhi vigezo ambavyo waandaji wamejiridhisha navyo.
Hayo
yameelezwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda alipokuwa anatoa
mada katika semina maalum kwa waandishi wa habari kuhusu uenyeji wa Mkutano
huo.
Semina hiyo
inayofanyika kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Januari 5, 2025
imefunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye aliwaomba waandishi wa habari
kutumia vizuri kalamu na sauti zao kutangaza mkutano huo na fursa zake kwa
wananchi.
Balozi Kaganda
alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa ni moja ya nchi chache za
Afrika zenye mipango thabiti ya kuwa na nishati ya kutosha na uhakika, mpango
wa kusambaza umeme nchi nzima ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji.
Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia, mikakati kabambe ya upatikanaji wa nishati ambapo malengo ifikapo 2030
asilimia 75 ya Watanzania wawe wamefikiwa na umeme na asilimia 80 wawe
wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034
Sababu
nyingine alizozitaji kuwa ni kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania, amani na
usalama na uzoefu wa kutosha wa kuwa nwenyeji wa mikutano mikubwa ambayo
imekuwa ikifanyika nchini.
Mkutano huo
unaondaliwa kwa ushirikiano baina ya Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya
Afrika, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Tanzania unalenga kuwakutanisha wakuu
wa nchi zote za Afrika na wadau wengine ili kujadili kwa pamoja njia za
kuchagiza upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa kutumia rasilimali
zilizopo.
Mkutano huo utakaofanyika
jijini Dar Es Salaam Januari 27 na 28, 2025 utahitimishwa kwa nchi 14 kusaini
Mpango wa Nishati ambao ni ahadi ya Serikali zao kuchukua hatua mbalimbali za
kufikisha umeme kwa wananchi.
Nchi hizo ni
Tanzania, Liberia, Senegal, Niger, Nigeria, Chad, Mauritania, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, Côte d’Ivoire, Burkina Faso, Malawi, Msumbiji na Zambia.
Mkutano huu
unaojulikana kwa kifupi kama Mission300 utajiwekea malengo ya kuwafikishia
umeme watu milioni 300 kati ya watu milioni 685 wanaoishi bila umeme barani
Afrika, ifikapo mwaka 2030.